Kocha wa timu ya taifa ya Ghana Avram Grant, wamewataka wachezaji wake kuwa na nidhamu ya mchezo watakapokua kwenye hekaheka za kusaka nafasi ya kutinga kwenye hatua ya fainali siku ya Al-Khamisi.

Grant ametoa wito huo kwa wachezaji wake, kufuatia mapungufu ya kujiamini kupita kiasi aliyoyaona kwenye michezo iliyopita, ambapo anaamini hali hiyo ilikua chanzo cha kuwa na wakati mgumu wa kupata ushindi mbele ya Congo DRC.

Amesema wachezaji wake wanapaswa kufahamu hakuna timu ndogo katika mashindano makubwa kama ya AFCON, hivyo ni wajibu wao kupambana na kutoona wana uwezo wa kumshinda kila wanaekutana nae.

“Haipendezi kwa mchezaji kucheza kwa kujiamini huku akiidharau timu pinzani, nimekaa na kikosi changu na kuwaambia ukweli wa jambo hilo. Wanapaswa kubadilika na kuondoa hiyo dhana,”Alisema kocha huyo kutoka nchini Israeli.

“Sifahamu kwa nini tabia hiyo iliibuka kwa wachezaji wangu, lakini ninaamini kwa nilivyo zungumza nao kutakua na mabadiliko makubwa katika mchezo wetu dhidi ya Cameroon.”

Timu ya taifa ya Ghana inawania taji la tano la michuano ya Afrika, na kwa mara ya mwisho walitwaa ubingwa huo mwaka 1982.

Anna Abdallah awataka viongozi wanawake kuwapa somo watoto wa kike
Manolo Gabbiadini Kumalizana Na Southampton