Waziri wa Maji,  Jumaa Aweso ameagiza kuondolewa katika wizara hiyo mhandisi wa maji wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) Wilaya Hanang,  Herbert Kijazi baada ya kuisababishia hasara Serikali ya Sh609 milioni.

Amesema kuwa Mhandisi Kijazi amesababishia hasara kwa Serikali  kwa kuruhusu ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mkoka Wilaya ya Kongwa wakati ripoti ya maabara ikionyesha kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuwa na chumvi nyingi.

Aweso ametaka meneja wa Ruwasa mkoani Dodoma, Godfrey Mbabaye na meneja wa Wilaya ya Kongwa,  Kaitaba Rugakingira kujieleza kwake kwa nini wasifukuzwe kazi kwa kutaka kusababisha hasara nyingine baada ya kumweleza kuwa wanahitaji Sh360 milioni.

Aweso amefanya ziara katika kijiji hicho na kusikiliza kero za wakazi wa eneo hilo ambapo wammueleza kuwa maji hayo yana chumvi na hayafai kwa matumizi yoyote ya binadamu.

Kauli za wananchi hao zilimfanya Aweso aagize kupigiwa simu kwa Kijazi na alipoulizwa kama ripoti ya maabara ilionyesha nini kabla ya utekelezaji wa mradi huo,  alijibu kuwa ilionyesha kuwa maji hayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu.

”Amesababisha hasara kwa Serikali, ujumbe umfikie katibu mkuu ( Anthony Sanga) kuwa huyu mhandisi hana kazi hapa wizarani,” amesema Aweso.

Watoto Nigeria watekwa nyara
Kahata anukia Azam Complex