Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekagua maendeleo na kupokea mabomba kwa ajili ya mradi wa maji Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema mradi huu ni wa haraka na utendaji wake ni wa tofauti na fedha zake zitoke kwa haraka kwani wananchi wanataka maji.
Aweso ameyasema hayo, baada ya kubainika uwepo wa Bonde lenye maji mengi ukanda wa Nzuguni DUWASA imechimba visima vitano (5) vyenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 7.6 kwa siku ambapo Maji yaliyopatikana yataongeza uzalisha kutoka lita million 68.6 hadi 76.2 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 11.7 kutoka kwenye uzalisha wa sasa.
Amesema, Mradi huo utawanufaisha wananchi wa Nzuguni, Kisasa, Ilazo na Swawa na kwamba tayari mabomba yameshafika na ni vyema kisiwepo kisingizio cha mkandarasi kukosa fedha ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma – DUWASA, Mhandisi Aron Joseph ahakikishe vifaa vinafika kwa wakati ili mabomba hayo yasambazwe na wananchi wapate huduma ya maji na kuishauri timu ya Rasilimali za Maji kufanya utafiti wa ziada ili kupata maeneo mengine yenye maji ya kutosha pembezoni mwa jiji la Dodoma, ili visima viongezwe na wananchi wapate huduma hiyo kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Nzuguni utakaowanufaisha wakazi 37,929 unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu (2023).
Amesema, mradi huo wenye mikataba minne yenye thamani ya Shilingi 4.8 Bilioni 4.8 hadi sasa DUWASA imepokea Shilingi 346.6 Milioni 346.6 kati ya Shilingi 1.8 Bilioni za malipo ya awali ya mradi na kwamba fedha zote zimepokelewa na zimelipa wakandarasi wa awali akiwemo wa ujenzi wa tenki.