Waziri wa Maji, Juma Aweso amewaonya Wahandisi na Wakandarasi wa maji kutokuchezea miradi ya maji na kuisimamia kwa umakini ambapo amesema yeyote atakayefanya hivyo atashughulikiwa ipasavyo.

Waziri Aweso ameyasema hayo leo Aprili 12, 2021 bungeni jijini Dodoma katika Bunge la 12, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Saba wakati akijibu swali la Mbunge Ester Bulaya, lililohoji nini chanzo cha miradi ya maji kutokukamilika kwa wakati au ikikamilika kutokutoa maji.

“Kubwa ambalo nataka niwaelekeze Wahandisi wa maji pamoja na Wakandarasi vipo vya kuchezea ukishiba chezea kidevu chako au kitambi chako lakini sio miradi ya maji, tutakushughulikia ipasavyo,” amesema Aweso.

Waziri Aweso amekiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya usimamizi wa miradi ya maji ambapo amelishukuru Bunge kwa kuliona hilo tatizo na kulitatua kwa kuwa na wakala wa maji vijijini, RUWASA.

Tayari Wizara ya Maji imeshaainisha miradi zaidi ya 177 na RUWASA imeshaanza kuitatua miradi hiyo zaidi ya 85.

Pia Waziri Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji imehakikisha Wahandisi wote wa maji waliokuwa chini ya Halmashauri wanakuwa chini ya Wizara.

Asante Namungo FC kwa kushiriki! Karibuni siku nyingine
Lwandamiza atuma salamu Young Africans