Waziri wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso ametuma salamu kwa makandarasi na wahandisi wa maji akiwataka wakae mguu sawa kwani kazi inakuja.
Ameeleza hayo bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Aprili 23, 2021 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dkt. Pius Chaya aliyehoji ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Kintingu – Lusilile ili wananchi wa vijiji 11 vya kata ya Chikuyu, Makutupora, Maweni na Kintinku waanze kupata maji safi na salama.
Kuhusu mradi huo, Aweso amekiri kuwa imechukua muda mrefu kukamilika lakini tayari wamemlipa mkandarasi na kumtaka afanye kazi kwa kasi inayotakiwa.
Awali Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema mradi wa maji Kintinku/Lusilile ni mradi mkubwa ambao unatekelezwa kwa awamu nne na hadi Machi 2021, 2021 utekelezaji wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 90.
Amesema zimeshatumika Sh2.085 bilioni na kwamba kazi zilizofanyika ni ufungaji wa mitambo ya kusukuma maji, ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukuma maji, tanki la kukusanya maji la lita 300,000 na ujenzi wa tanki la kuhifadhi na kusambaza maji la lita 2 milioni.
Pia, ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilomita 1.2 ambapo vijiji vitatu vya Chikuyu, Mwiboo na Mbwasa vinatarajiwa kuanza kupata huduma ya maji Juni 2021.