Beki wa Manchester United, Axel Tuanzebe anatarajiwa kurejea kwenye klabu ya Aston Villa kwa mkopo, kwa mara ya pili mfululizo.
Beki huyo wa kati, aliondoka Old Trafford mwezi Januari mwaka huu na kujiunga na Aston Villa ambapo alicheza michezo mitano ya ligi daraja la kwanza msimu wa 2017/18.
Tuanzebe mwenye umri wa miaka 20, amekua na kikosi cha Man utd wakati wote wa michezo ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi, na ameonyesha kiwango kikubwa.
Aston Villa pia wana mpango wa kumsajili kiungo wa klabu ya Millwall George Saville lakini wanakabiliwa na upinzani kutoka kwenye klabu ya Leeds Utd.
Klabu hiyo ya Villa Park, pia inatarajia kufanya biashara ya kumuuza kiungo mshambuliaji Jack Grealish, baada ya kupokea ofa kutoka Tottenham.
Meneja wa Spurs, Mauricio Pochettino amevutiwa na kiwango cha kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 na anatarajia kukamilisha uhamisho wake kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili juma hili.
Katika hatua nyingine mchezaji mwingine wa Man Utd Demetri Mitchell anatarajiwa kupelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Heart of Midlothian F.C ya Scotland.
Mitchell alipata nafasi ya kukuza na kuendeleza kipaji chake alipokua na klabu hiyo kwa mkopo msimu uliopita, na viongozi wa klabu hiyo wameona kuna haja ya kumrejesha ili kupata huduma yake kwa mara nyingine tena.