Beki wa kati wa Manchester City, Aymeric Laporte ametangaza kuondoka katika kikosi cha klabu hiyo na kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Laporte amekamilisha mpango wa kusajiliwa na klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia, baada ya kudumu Manchester City kwa miaka mitano na nusu.

Raia huyo wa Hispania, ameripotiwa kuwekewa dau nono na timu hiyo ya Saudi Arabia akimfuata Riyad Mahrez alisajiliwa katika kikosi cha Al-Ahli mwezi uliopita.

Katika mtandao wake wa Twitter, mchezaji huyo aliwaaga mashabiki wa Manchester City na kusisitiza kwamba amekwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.

“Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwaaga mashabiki wa soka wa Manchester City kwa kunipa sapoti katika kipindi chote nilichokuwa ndani ya kikosi hicho.

“Ninawashukuru wachezaji wenzangu na viongozi kwani mliishi na mimi kama familia moja kwa kipindi chote mlinionyesha upendo wa hali ya juu.

“Umefika wakati wa mimi kuondoka katika kikosi cha Manchester City na kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine nitawakumbuka daima,” amesema.

Laporte anaondoka Etihad baada ya kucheza mechi 180 za Manchester City ukiwemo mchezo uliopita dhidi ya Burnley.

Mchezaji huyo alipata mafanikio makubwa ndani ya kikosi hicho kwa kushinda mataji 13 ikiweno mataji matano ya Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Putin avunja ukimya kifo cha Bosi wa Wagner
Ahmed Ally: Hatutaki kufungwa fungwa