Klabu ya Manchester City imemsajili beki wa Ufaransa Aymeric Laporte kutoka Athletic Bilbao kwa kitita kilichovunja rekodi ya timu hiyo cha £57m.
Kitita hicho cha Laporte kinafanya gharama za usajili kwa vilabu vya Uingereza mwezi huu kufikia £252m ikiwa ni rekodi katika uhamisho wa mwezi Januari.
Kuwasili kwa mchezaji huyo ,mwenye umri wa miaka 23 kunajumlisha gharama ya klabu hiyo kuwanunua mabeki tangu mwisho wa msimu uliopita kufika £215.5m.
Rekodi ya awali iliwekwa na kiungo wa kati wa klabu hiyo Kevin de Bryune aliyenunuliwa kwa kitita cha £55m mwaka 2015.
”Ninatazamia kufanya kazi chini ya mkufunzi Pep Guardiola na kujaribu kuisaidia klabu hiyo kupata ufanisi. Inamaanisha kwamba klabu hii imeniamini na nafurahia kushirikiana nayo,” amesema.
Wasiwasi kuhusu jeraha la beki Vincent Kompany mbali na wasiwasi mwingine kuhusu kutokuwepo kwa Eliaquim Mangala kumemshinikiza Kocha Guardiola kuamini anahitaji beki mwingine wa kati mbali na John Stones na Nicolas Otamendi.