Mshambuliaji wa Tanzania na klabu ya Coastal Union Ayoub Lyanga amesema klabu ya Young Aficans imekua ikionyesha nia ya kumsajili kila unapofika wakati wa usajili, lakini nia yao haitimii.
Mshambuliaji huyo tegemezi kwenye kikosi cha Coastal Union amesema misimu miwili mfululizo klabu hiyo ya jijini Dar es salaam, viongozi wake wamekua wakionyesha nia ya kumsajili lakini hawamalizi lengo lao.
Amesema taarifa za kuhitajika Young Africans amekua akielezwa na meneja wake Jamal Kisongo, ambaye mara zote alishirikishwa kwenye mazungumzo ya awali.
“Ndio kweli, misimu miwili Young Africans wanaonesha nia ya kunisajili ila wanaishia mitini hata msimu huu pia wamekuja wameongea na meneja wangu Jamal Kisongo na mazungumzo yalikuwa mazuri.” Alisema mshambuliaji huyo.
Katika hatua nyingine Ayoub Lyanga amesema huenda akatimkia nchini Serbia, kufuatia klabu ya Macva FC kuonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
“Kwa sasa hivi kuna klabu ya Macva FC kutoka Serbia inayoshiriki ligi kuu nchini humo inataka nikafanye nao kazi.”
“Ndoto yangu ilikuwa kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, nina amini hii ndio safari yangu tusubirie tu Janga la Corona kupita, kila jambo litakuwa sawa”. Alisema Lyanga.