Wachezaji wa wa Azam FC hawataki kupoteza kwa mara ya pili dhidi ya Young Africans watakapokutana katika mchezo unaofuatia wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24.
Timu hizo zilivaana hivi karibuni katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani uliomalizika kwa Young Africans kushinda mabao 2-0.
Young Africans na Azam FC zitakutana tena Oktoba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam katika mchezo wa ligi unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe amesema kuwa wachezaji wote wana morali kubwa kuelekea mchezo huo wa ligi, ambao wameahidi kulipa kisasi cha kufungwa.
Ameongeza kuwa wanapata jeuri ya kupata ushindi katika mchezo huo baada ya kurejea kwa mshambuliaji wao tegemeo Mzimbabwe, Prince Dube ambaye ataingia uwanjani akiwa fiti asilimia 100 akitokea katika majeraha.
“Young Africans walitufunga katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii kutokana na timu kukosa muunganiko wa haraka, tukiwa katika Pre Seasson msimu huu.
“Sasa hivi tayari timu imeungana kwa wachezaji kucheza kitimu, hivyo katika mchezo huo tutaingia kwa lengo moja pekee la ushindi na sio matokeo mengine.
“Uzuri ni kwamba wachezaji wenyewe wameonekana kuitaka mechi, kwa lengo la kulipa kisasi katika mchezo huo ni baada ya kuchukizwa na matokeo waliyoyapata katika mchezo wa Ngao ya Jamii,” amesema lbwe