Baada ya kumalizana na Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ akitokea Young Africans, mabosi wa Azam FC sasa wanapambana kuhakikisha wanamsajili Mlinda Lango wa Geita Gold, Arakaza Macarthur raia wa Burundi ili kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu na mshindano ya kimataifa.
Mlinda Lango huyo mkataba wake na Geita Gold unaelekea ukingoni na viongozi wa Geita wanapambana kutaka kumbakisha licha ya nia ya Azam FC ya kumtaka Mrundi huyo.
Habari za uhakika zinaeleza Azam FC tayari wameshafanya mazungumzo na Mlinda Lango huyo ambaye ameonyesha nia ya kutaka kujiunga na timu hiyo licha ya mabosi wake kupambana katika kuhakikisha anabakia kwa ajili ya msimu ujao.
“Ni kweli Arakaza anatakiwa na Azam FC kutokana na kiwango chake ambacho amekionyesha msimu huu, lakini hata Geita wenyewe kwa sasa wanamekuwa wakipambana kuhakikisha anabakia kwenye timu yao ili kuweza kutimiza malengo yao ya kufanya vizuri msimu ujao,” amesema mmoja wa watu wa karibu wa Arakaza
Aidha, mtoa habari huyo amesema licha ya klabu hizo kupambana kutaka kumsajili, Mlinda Lango huyo pia ana ofa mbili kutoka mataifa ya kiarabu wanamtaka.
Hata hivyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Geita Gold FC, Leonard Bugomora, amesema wamesikia tetesi za Mlinda Lango huyo kutakiwa na Azam, hata hivyo hawako tayari kupoteza wachezaji wao muhimu na Arakaza ni mmoja wao.
Amesema kamati ya utendaji ya klabu hiyo itakutana siku yoyote kuanzia sasa kufanya tathmini ya ligi iliyomalizika na kujadili mipango ya msimu ujao wa 2023/24.
“Tunatarajia kukutana kamati ya utendaji kupitia ripoti ya benchi la ufundi na kuona wachezaji ambao wamemaliza mikataba yao kuongezewa hasa wale waliokuwa kikosi cha kwanza, tunahitaji kuimarisha timu yetu, tunatambua kuna baadhi ya wachezaji wetu wanawindwa na baadhi ya klabu akiwamo huyo kipa wetu (Arakaza), tunaamini tutawabakisha,” amesema Bugomora.
Ameongeza kuwa baada ya kamati ya utendaji kukutana na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwamo tathmini ya kikosi cha timu yao na wafanye nini kwa msimu ujao watawasilisha kwenye Bodi ya wakurugenzi ya timu hiyo.