Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kuelekea Cairo, Misri leo Jumatano (Oktoba 20) jioni, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili wa kombe la Shirikisho hatua ya kwanza dhidi ya Pyramids FC.
Wachezaji 25 na Waafisa wa Benchi la Ufundi wataondoka jijini Dar es salaam wakiwa na lengo la kwenda ugenini kupambana, baada ya kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya miamba hiyo ya soka Barani Afrika.
Mchezo wa mkondo Pili kati ya Azam FC dhidi ya Pyramids FC umepangwa kucheza kwenye uwanja wa June 30, Jumamosi (Oktoba 23) mishale ya saa nne usiku.
Azam FC itapaswa kusaka ushindi ama matokeo yoyote ya sare ya mabao, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku wenyeji wao wakihitaji ushindi pekee ambao utawavusha.