Klabu ya Azam FC huenda ikapanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara endapo itaifunga Dodoma Jiji FC, katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa baadae leo Jumanne (Oktoba 03) Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti, Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa wakati wenyeji wa mchezo huo, Dodoma Jiji wapo nafasi ya saba kwenye msimamo wakikusanya pointi nne timu zote mbili zikicheza mechi tatu.
Endapo Azam FC itashinda mchezo wa leo itafikisha pointi 12 na kuwashusha kileleni mwa msimamo mabingwa watetezi Young Africans, ambao kwa sasa ndio vinara wakilingana na Azam FC pamoja na Simba SC iliyopo nafasi ya pili, lakini wenyewe wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga.
Kuelekea mchezo huo kila upande umetamba kuibuka na ushindi ambapo Kocha Msaidizi wa wenyeji Dodoma Jiji, Kassim Liogope amesema wamejiandaa kukabiliana na wapinzani wao wakijua ni timu kubwa yenye malengo ya kushinda.
“Tunatambua ubora wao na sisi benchi la ufundi tumewaandaa vijana wetu kuhakikisha tunawadhibiti na kupata ushindi, tunajua watakuja kulipa kisasi baada ya kuwafunga msimu uliopita lakini tupo imara kuhakikisha tunaendeleza ubabe,” amesema Liogope.
Kwa upande wa Azam FC, Kocha Msaidizi, Bruno Ferry amesema itakuwa mechi ngumu kwa timu zote mbili, wanawaheshimu Dodoma Jiji kama ilivyo kwa timu nyingine zilizopo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.