Kikosi cha Azam FC kitacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Gor Mahia FC ya Kenya, kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia msimu huu, pamoja na mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Mtibwa Sugar.
Azam FC imethibitisha uwepo wa mchezo huo kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii, baada ya Benchi la Ufundi kupendekeza kuchezwa kwa michezo hiyo angalau miwili katika kipindi hiki cha Kalenda ya FIFA.
Mchezo huo dhidi ya Gor Mahia umepangwa kuchezwa Jumamosi (Machi 26) katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya.
Kabla ya mchezo huo Azam FC itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya JKU kutoka visiwani Zanzibar keshokutwa Jumatano (Machi 22), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Benchi la Ufundi Azam FC Dani Cadena amesema wamelazimika kukitumia kipindi hiki kwa mchezo huo, ili kuwaweka sawa wachezaji wao waliosalia kikosini, baada ya wenzao kumeitwa kuziwakilisha timu zao za taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Cadena amesema kutakuwa na muda mrefu kwa wao kutocheza, hivyo wameona ni vyema kutotoa ruhusa ya mapumziko kwa lengo la kurejesha morali ya timu yao baada ya kusuasua hivi karibuni.
“Ruhusa ambayo tumeitoa ni kwa wachezaji walioitwa timu za taifa, wengine wote tutaendelea na mazoezi kwa lengo la kujiweka imara zaidi kutokana na michezo migumu iliyokuwa mbele yetu,” amesema Dani Cadena
Mchezo wa mwisho kwa Azam FC ulikuwa ni Machi 13 ilipochapwa bao 1-0 na Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estate na baada ya hapo itacheza na Mtibwa Sugar katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kati ya Aprili 1-6.
Wachezaji Raia wa Tanzania, Sospeter Bajana na Abdul Suleiman ‘Sopu’ ni wachezaji wa Azam FC walioitwa katika kikosi cha ‘Taifa Stars’ kilichoelekea Misri tayari kwa mchezo wa kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Uganda.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Machi 24 nchini Misri, kabla ya timu hizo hazijarudiana jijini Dar es salaam Machi 28.