Kikosi cha Azam FC leo Jumatatu (Novemba 30) kitarejea dimbani kusaka alama tatu muhimu za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United Mara, kwenye uwanja wa Karume mjini Mumsoma-Mara.

Azam FC watashuka kwenye dimba hilo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwiwli mfululizo dhidi ya KMC FC na kisha Young Africans, yote wakicheza Dar es salaam.

Kutokana na mazingira hayo, Azam FC inatarajiwa kuutumia mchezo wa leo Jumatatu (Novemba 30) kama sehemu ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye michezo hiyo miwili na kusababisha kutimuliwa kwa kocha Aristica Cioaba.

Kaimu kocha mkuu wa Azam FC Vivier Bahati, amesema tayari vijana wake wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo, na anatumai watapambana ndani ya dakika 90 na kupata matokeo ya kuridhisha.

“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Biashara United Mara, nina uhakika wachezaji wangu wataonyesha soka la ushindani, ambalo litatupa matokeo mazuri,”

“Tumekua na matokeo mabaya kwenye michezo yetu miwili iliyopita, jambo hili limetuumiza sana, hivyo hatutaki lijirudie tena kwenye mchezo wetu wa leo hapa Musoma.” Amesema Vivier Bahati.

Kwa upande wa Biashara United Mara, walipoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar kwa kufungwa mabao matatu kwa sifuri.

Nao watahitaji kushinda mchezo wa leso dhidi ya Azam FC ili kutuliza machungu walioyapata juma lililopita.

Azam FC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 25, wakitanguliwa na Young Africans wenye alama 31.

Biashara United Mara inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 18.

Maafisa mawasiliano Ikulu ya Marekani watajwa
UN yakanusha idadi ndogo waliouawa Nigeria