Kikosi cha Azam FC kesho Ijumaa (Julai 14) kinatarajia kucheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki tangu itue Tunisia kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Azam FC imepanga kucheza mechi nne za kirafiki na kesho itaanza kwa kucheza na dhidhi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Azam FC itakipiga na timu hiyo ambayo msimu uliopita ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa Young Africans, lakini baada ya hapo inatarajiwa kucheza mechi zingine tatu dhidi ya timu za CS Sfaxien, US Monastir na Esperance zote za Tunisia.
Akizungumza kutoka kwenye Jiji la Sousse nchini humo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hasheem Ibwe amesema kupata mechi za kirafiki na timu zinazocheza mechi za kimataifa ndiyo ilikuwa dhamira yao kwenda kuweka kambi nchini humo.
Tunategemea siku ya Ijumaa (kesho) kucheza mchezo wa kwanza wa kujipima nguvu na hii ni dhamira tulioiweka tangu tuko Dar es Salaam kwamba tutacheza mechi za kirafiki za hadhi ya klabu ambazo huenda tukakutana nazo kwenye michuano ya kimataifa lakini zitatuweka vizuri kujiandaa na timu za nyumbani, tunatarajia kuanza kucheza na Al Hilal Omdurman ya Sudan baada ya hapo kuna michezo mingine mitatu tutacheza, mechi hizi zitatoa nafasi kwa benchi letu la ufundi kuangalia nini cha kufanya,” amesema Ibwe.
Akizungumzia kambi, amesema inakwenda vyema na tayari shughuli iliyokuwa inakusudiwa na Kocha Msenegal, Youssouph Dabo, imeshaanza na amekuwa akitoa dozi kwa wachezaji wake ili kutegeneza kikosi imara.
“Kikosi kiko kwenye hali nzuri, walipofika walifanya mazoezi ya kutoa uchovu baada ya safari ndefu, lakini ile shughuli pevu imeshaanza ya kujiandaa na msimu mpya kila mchezaji ameonyesha utayari, kujituma na kuonyesha kuwa anastahili kuwa kwenye sehemu ya kikosi cha mwalimu na hata mwenyewe ameridhishwa na kile kinachofanywa na wachezaji wake na ameanza kutoa dozi kwa ajili ya kukifanya kikosi kiwe imara,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Ibwe, amelisifu eneo na hoteli waliyofikia kuwa ni sehemu nzuri yenye utulivu, huku akisema hoteli hiyo ina kila kitu kinachohitajika na wachezaji wao hawalazimiki kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya mazoezi.