Baada ya kumshusha mshambuliaji kutoka DR Congo Mpiana Monzizi akitokea FC Lupopo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, Uongozi wa Azam FC umepania kushusha majembe mengine ili kukidhi hitaji la kocha mkuu George Lwandamina.
Azam FC imekua na mendelezo kupata matokeo mabaya kwenye michezo ya Ligi Kuu kwa siku za karibuni, hali ambayo imelifanya benchi la ufundi kuwasilisha mapendekezo ya kuongeza nguvu kwenye kikosi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Zakaria Thabit (Zaka Zakazi) amesema kocha mkuu George Lwandamina amependekeza usajili wachezaji kati ya wawili ama watatu ambao anaamini watafanikisha lengo la kukiongezea nguvu kikosi chake, katika harakati za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC).
“Sifa ya timu kubwa ni kufanya usajili nasi pia lazima tufanye usajili kwenye hili dirisha dogo, mashabiki wasiwe na mashaka ripoti inaeleza kila kitu.
“Ninadhani tutahitaji wachezaji wawili ambao watakuwa na kazi ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chetu ila kuhusu Perfect bado sijajua kama anahitajika na Azam FC.” Amesema Zaka Zakazi.
Azam FC ambayo Jumamosi (Desemba 26) ilishinda mchezo wake wa ASFC dhidi ya Magereza FC na kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 29, ikitanguliwa na mabingwa watetezi Simba SC wenye alama 32, na Young Africans ipo kileleni ikiwa na alama 43.