Uongozi wa Azam FC umetamba kufanya kufuru kwenye dirisha kubwa la usajili kwa kushusha washambuliaji wawili kutoka nchi za Ivory Coast na Ghana.
Kaimu Msemaji wa Azam FC, Hashim Ibwe amesema watawatambulisha wafumania nyavu hao wawili siku chache kabla ya msimu wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara kumalizika mwezi Juni.
“Lengo letu msimu ujao ni kubeba makombe yote ya ndani lakini pia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika angalau tuvuke hatua ya makundi sababu tumepanga kuja kivingine zaidi,” alisema Ibwe ambaye hakutaja majina ya washambuliaji hao.
Amesema mchakato wa kuboresha kikosi chao walishauanza mapema hiyo ni kutokana na bosi wao mkuu, Yusufu Bakhressa pamoja na uongozi wa juu kuamini kwamba wana uwezo wa kufanya vizuri kama watafanya usajili wa nguvu.
Ibwe amesema wamepanga kusajili wachezaji watatu pekee kwenye dirisha kubwa wameanza na wawili na baadaye watamaliza na mchezaji mmoja anayecheza nafasi ya kiungo wa chini na kisha baada ya hapo wataweka wazi majina ya wachezaji ambao wataachana nao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mikataba kumalizika na kushuka kiwango.