Kikosi cha Azam FC kinatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Jumatatu (Oktoba 09) kikitokea Libya, kilipokuwa kimekwenda kucheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Al-Akhdar.
Azam FC inarejea nyumbani ikiwa kichwa chini baada ya kufungwa mabao 3-0, hali ambayo itawalazimu kusaka ushindi zaidi ya mabao 3-0 kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumapili (Oktoba 16).
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema wanarejea nchini wakiwa na matumaini ya kupambana na kupata matokeo yatakayowavusha kwenda hatua inayofuata.
“Tumepoteza mchezo wa ugenini, tuna nafasi ya kucheza nyumbani mwishoni mwa wiki hii, ninaamini kikosi chetu kitaandaliwa vizuri, na kupata matokeo,”
“Tunaamini Kocha wetu Lavagne ameona makosa yaliyofanyika hadi tukapata matokeo ya kupoteza, atayafanyia baada ya kurejea nyumbani, In Shaa allha ninaamini tutafanya vizuri katika mchezo wa marudiano.” amesema Popat
Tayari Azam FC itashuka dimbani Jumapili (Oktoba 16) ikiwa na kaulimbiu yake ya Inawezekana! Tukutane Azam Complex Oktoba 16.