Klabu ya Azam FC imesema inatarajia kujinoa kwa michezo miwili ya mwisho ya maandalizi ya msimu wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa dhidi ya Stade Tunis na Club Africain za Tunisia.

Azam FC inatarajia kuhitimisha kambi ya majuma matatu nchini humo na pengine juma lijalo itarejea kujiandaa na michezo ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Tayari timu hiyo imeshacheza michezo mitatu ya kirafiki ikiwa huko dhidi ya US Monastir iliyoshinda mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikishinda mabao 3-0 na kupoteza mabao 3-0 dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Akizungumza nchini Tunisia, Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe amesema kwa sasa kocha wa kikosi hicho, Youssouph Dabo amekuwa akitaka kuona kwa vitendo mbinu wanazofundishwa wachezaji.

“Mbinu zote walizofundishwa wamekuwa wakizifanya kwa vitendo uwanjani kwa kujipima na timu kubwa ili kujua nguvu na udhaifu na kuyafanyia kazi na baada ya michezo mitatu, tutacheza mingine miwili ya kuhitimisha,” amesema.

Ibwe amesema michezo hiyo ijayo watacheza Julai 26 na 27 kisha watakuwa imara kurejea kumalizia kambi nyumbani kwa hatua za mwisho za kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii uliopo mbele yao, ambapo wanatarajia kucheza na Young Africans.

Pochettino aweka matumaini kwa Levi Colwill
Kombaini ya Songwe kuipima Tanzania Prisons