Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkareem Amin ‘Popat’ amekiri kupokea Ofa ya Young Africans inayosisitiza usajili wa Kiungo kutoka nchini Ghana James Akaminko.
Young Africans jana Jumatano (Desemba 28) ilithibitisha kutuma ofa ya kutaka kumsajili kiungo huyo, ambaye amekua na kiwango kizuri tangu alipoanza kuonekana katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Azam FC msimu huu 2022/23.
Popat amesema ni kweli Young Africans wamewasilisha ofa yao, na Uongozi wa Azam FC umepanga kutoa majibu kamili baada ya juma moja, kwa sababu wanaamini Mchezaji yoyote ana haki ya kuuzwa na kusajiliwa.
Amesema baada ya mchezo wao dhidi ya Mbeya City ambao utachezwa mwishoni mwa juma hili Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, Uongozi wa Azam FC utakutana rasmi kujadili ofa ya Young Africans na kutoka na majibu ambayo yatarudishwa kwa wahusika.
“Tumepokea barua yao na tumeshawajibu. Ndani ya siku saba tutawaambia tulipofikia. Duniani hakuna mchezaji ambaye hauzwi.”
“Tukimaliza mechi yetu na Mbeya City tutakaa pamoja na viongozi kujadili biashara hii. Timu yetu inajitosheleza sana na hatuna mahitajio ya mchezaji yeyote mpya kwa sasa ” amesema Popat
Azam FC ilimsajili James Akaminko akitokea Ashanti Gold FC ya nyumbani kwao Ghana, mwanzoni mwa msimu huu na hadi sasa amekua muhimili mkubwa katika idara ya kiungo mkabaji.