Klabu ya Azam FC imetamba kuwa na mikakati mizuri kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utaanza rasmi mwishoni mwa juma hili kwenye viwanja tisa tofauti.
Azam FC walimaliza kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20, huku wakipishana alama mbili na Young Africans waliomaliza nafasi ya pili kwa kumilik alama 72, huku Simba wakitwaa ubingwa VPL kwa mara ya tatu mfululizo.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema wamejipanga vema na wana mikakati imara kuhakikisha wanapigania ubingwa wa VPL ambao pia unawaniwa na klabu kongwe za Simba na Young Africans, zote za jijini.
Bahati amesema timu yake ina kiu na taji hilo ambalo waliwahi kulichukua mara moja katika msimu wa 2013/14, na sasa wanafikiri ni wakati sahihi kurejea klabuni hapo.
“Tumejipanga imara, tumeyafanyia kazi mapungufu ya msimu uliopita, tumekuwa na maandalizi mazuri, kwa kifupi tunahitaji kushinda taji la Ligi Kuu Tanzania, tumedhamiria kuusaka ubingwa kwa udi na uvumba,” amesema Bahati.
Kocha huyo ameongeza usajili waliofanya umelenga kuwania ubingwa na ulifuata mapendekezo ya ripoti ya kiufundi waliyoiwakilisha kwa viongozi baada ya kumaliza msimu uliopita.
Amesema viongozi walikamilisha majukumu yao kwa upande wa utawala na kazi imebaki kwao wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha malengo yanatimia.
“Tunaendelea na programu ya mazoezi tuliyoiandaa, inakwenda vizuri kwa sababu tunataka kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika michezo yetu yote ya ligi ya msimu huu, najua itakuwa ni ligi yenye ushindani mkubwa, kwa sababu kila timu imejipanga na kujiimarisha vizuri,” amesema Bahati.
Katika kujiandaa na msimu mpya, Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo ya Lindi halafu ikawafunga KMC bao 1-0 na vile vile ililazimishwa sare ya goli 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Azam Complex.
Azam FC wataanza msimu wa 2020/21 nyumbani kwa kuwakaribisha Polisi Tanzania kutoka Kilimanjaro, Moshi wakati mabingwa watetezi watakuwa ugenini Mbeya kuwakabili Ihefu FC huku Tanzania Prisons wakiwafuata Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salam.