Baada ya kufika salama mjini Songea mkoani Ruvuna jana Jumatano (Juni 23), na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki waliojitokeza Uwanja wa ndege, Uongozi wa Azam FC umetoa neno la shukurani kwa ukarimu walioupata.

Azam FC waliwasili jana mchana mjini Songea, tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), utakaowakutanisha dhidi ya Simba SC, Jumamosi (Juni 26) Uwanja wa Majimaji.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Azam FC, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema wamefurahishwa na mapokezi walioyapata kutoka kwa mashabiki wao huko mjini Songea mkoani Ruvuma.

“Mapokezi ambayo yamefanywa na mashabiki wetu hapa Songea ni makubwa na kila mmoja ameweza kuona namna gani tunapendwa kila kona.”

“Ukweli ni kwamba tunawashukuru mashabiki kwa namna ambavyo wametupokea na tunaomba waendelee na sapoti yao bila kuchoka,” amesema Zaka Zakazi.

Kikosi cha Azam FC jana kilifanya mazoezi mepesi mjini Songea ili kurejea kwenye ubora wao na leo pia wataendelea na mazoezi, ya kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba SC.

Mchezo mwingine wa Nusu Fainali ya michuano hiyo utachezwa kesho Ijumaa (Juni 25) mjini Tabora kati ya Young Africans dhidi ya Biashara United Mara, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.

Rais Mwinyi amteua Makamu wake kuwa Mwenyekiti Tume ya udhibiti Dawa za Kulevya
Waziri Bashungwa apokea ugeni kutoka Brazil