Uongozi wa Azam FC umekiri kikosi chao kimeteleza katika mbio za ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kupoteza michezo dhidi ya Polisi Tanzania, Biashara United Mara na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union.

Azam FC ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania na 2-0 dhidi ya Biashara United Mara, hali iliyoifanya klabu hiyo ya Jijini Dar es salaam kuangusha alama 08.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zacharia ‘ZAKAZAKAZI’ amesema kikosi chao kimekua na mwenendo wa kutokuridhisha kwa siku za karibuni, na hilo ni jambo la kawaida katika medani ya soka la ushindani.

Amesema Uongozi unaamini Benchi la Ufundi linayafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo hiyo, ili kurejea katika hali ya ushindani na kupata ushindi kwenye michezo itakayowakabili siku za karibuni.

“Hatujakuwa na matokeo mazuri katika michezo yetu ya hivi karibuni, kama ilivyokua wakati tunatoka kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi, tulicheza michezo mitatu ya Ligi Kuu na mmoja wa Kombe la Shirikisho, tulipata matokeo mazuri ambayo kila mmoja aliyafurahia.”

“Kuna msemo unasema ‘UNAPOANZA KUAMINI HUWA UNASAHAU KUSHINDANA’ hii imetutokea sisi Azam FC kwa sababu tuliamini tulifika tulipokua tunahitaji kufika, kumbe haikua hivyo, tunaamini Benchi la Ufundi lipo kazini linayafanyia kazi madhaifu yaliyotuangusha katika michezo tuliopoteza, ili kuondoa ile hali ya kujiamini kupita kiasi.

“Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Biashara hali ilibadilika, kila mmoja wetu ni kama alichanganyikiwa kwa sababu hakuna aliyetegemea matokeo yale, haya matokeo yalituharibu kisaikologia na kujikuta tukiendeleza hali ya kushindwa kufanya vizuri katika michezo miwili iliyofuata.” amesema ZAKAZAKAZI

Kwa hatua ya kushindwa kuwika katika michezo mitatu mfululizo, Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 25 sawa na Namungo FC, lakini ina uwiyano mdogo wa mabao ya kufungwa na kufunga.

Azam FC yasalimu amri Ligi Kuu Tanzania Bara
Kaseja akiri kucheza chini ya kiwango