Kikosi cha Azam FC kinaendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko watano wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, utakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Jumapili Oktoba 04.

Azam FC watakua na sababu ya kupambana vilivyo kwenye mchezo huo, ili kufanikisha lengo la kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kushinda michezo minne, ambayo imewafanya kufikisha alama 12.

Kocha msaidizi wa kikosi cha vinara hao wa Ligi Kuu Vivier Bahati amesema tangu waliporejea jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Rukwa, wamekua katika Program maalum ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar.

Kocha Bahati amesema Program wanayoendelea nayo kwenye maandalizi ya mchezo unaofuata, inawapa matumaini ya kufanya vizuri na kuamini watafikisha alama 15 mwishoni mwa juma hili.

Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Burundi amekiri mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakuwa na ushindani kwa sababu ya timu zote zinahitaji kupata matokeo, lakini bado akasisitiza Azam FC wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

Mbali na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, Azam FC wanajiandaa kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar, huku wakiwa na chagizo lingine la kuwa na mshambuliaji Prince Dube anaeongoza katika orodha ya wafungaji bora mpaka sasa.

Dube anaongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao matatu, akifuatiwa na Clatous Chama, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Muzamiru Yassin wote kutoka Simba SC, Hassan Kabunda, Reliant Lusajo (KMC), Marcel Kaheza (Polisi Tanzania), Lamine Moro (Young Africans) na Bigirimana Blaise wa Namungo FC.

Makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya kupangwa leo
John Legend na mkewe wapata Pigo