Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hivi sasa ipo safarini kuelekea mkoani Tanga kwa ajili ya kucheza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT ya huko keshokutwa.

Azam FC iliyoanza safari hiyo kutoka kwenye Makao Makuu yake, Azam Complex saa 5.30 asubuhi mara baada ya mazoezi, imeenda huko ikiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi ili kuendeleza vita ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu kama ilivyojipangia mpaka sasa wakilingana kwa pointi na kinara Yanga, wote wakiwa na pointi 36.

Kikosi cha Azam FC kilichoelekea huko kinaundwa na makipa Aishi Manula na Mwadini Ali, mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Waziri Salum, Said Morad ‘Mweda’, David Mwantika na Racine Diouf.

Viungo ni Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, Michael Bolou na Mudathir Yahya ‘Muda’.

Washambuliaji ni Nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche na Ame Ally ‘Zungu’.

Wachezaji walioshindwa kuambatana na timu hiyo ambao ni majeruhi ni beki Aggrey Morris mwenye maumivu ya goti huku Ramadhan Singano ‘Messi’ pamoja na washambuliaji Allan Wanga na Didier Kavumbagu wakisumbuliwa na majeraha ya enka.

Winga machachari Farid Mussa yeye amepewa ruhusa maalumu ya kwenda kumuuguza mama yake mzazi anayeumwa.

Ripoti: Asilimia 1 ya matajiri wanamiliki utajiri zaidi ya mali za watu wote duniani
TFF Wamlilia Seleman Said ‘Yeltisn’