Klabu ya Azam FC imejipanga kuisambaratisha Mbeya City FC kwenye mchezo wa mzunguuko wa 37 Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa keshokutwa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.
Azam FC wamejizatiti kufanya vyema katika mchezo huo, baada ya kuambulia alama moja kwenye michezo miwili iliyopita, wakianza na Mtibwa Sugar waliowachabanga bao moja kwa sifuri juma lililopita Mjini Gairo, kicha wakalazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Lipuli FC mwishoni mwa juma lililopita, mjini Iringa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Zakaria Thabit (Zaka Za Kazi) amesema wanahitaji ushindi na kikosi chao kipo tayari kwa ushindani dhidi ya Mbeya City, ambao wameanza safari kutoka mjini Mtwara, ambapo mwishoni mwa juma lililopita walicheza dhidi ya Ndanda FC.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamefikisha alama 66 wakiachwa na Young Africans kwa tofauti ya alama mbili.
Young Africans ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 68 zote zimecheza jumla ya michezo 36 ndani ya Ligi Kuu Bara na hesabu zao wote ni kuona wanamaliza wakiwa nafasi ya pili.
Azam FC inakutana na Mbeya City ambayo inapambana kubaki ndani ya Ligi, hivyo utakuwa ni mchezo wenye ushindani mwanzo mwisho.
Mbeya City iliyo chini ya kocha Amri Said ipo nafasi ya 13 ikiwa na alama 42 ambazo hazimpi uhakika wa kubaki ndani ya ligi ikiwa atapoteza kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Michezo mingine ya mzunguuko wa 37 Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa juma hili.