Kocha wa Azam FC, Kalli Ongala, amesema kikosi chake kitazishughulikia timu zote atakazokutana nazo kuelekea ukingoni mwa Msimu huu 2022/23, ikiwemo Ruvu Shooting itakayocheza nayo Jumamosi (April 22).
Azam FC imebakisha michezo minne msimu huu ambayo ni dhidi ya Ruvu Shooting, Namungo FC, Coastal Union na Polisi Tanzania.
Timu hiyo kutoka Chamazi jijini Dar es Salaam, inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 50 baada ya kushuka dimbani mara 26, imefunga mabao 41 na kuruhusu mabao 26.
Kocha Ongala amesema anaendelea kukinoa kikosi chake kwa mchezo ujao dhidi ya Ruvu na anaamini timu yake itapata ushindi.
Kocha huyo amesema kwa sasa mipango yake katika michezop iliyobakia kwani anahitaji kikosi chake kishinde yote ili kijiweke katika nafasi nzuri.
“Ligi ndiyo inaenda ukingoni na sisi tunataka kuhakikisha tunamaliza ligi kwa kukaa katika nafasi nne za juu ili tuweze kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao,” amesema Ongala.
Kocha huyo ameongeza kuwa kwa sasa wachezaji wake vyema kisaikolojia kuhakikisha wanapata ushindi katika michezo yote ijayo wakianza na Ruvu Shooting.