Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, ameonyesha kuzihitaji pointi tatu za Azam FC, timu ambayo watakutana nayo wiki ijayo katika Ligi Kuu Bara, hiyo ni baada ya kuwapa wachezaji wake mazoezi ya nguvu kuhakikisha wanafanikiwa kushinda katika mchezo huo.

Simba ambayo ipo nafasi ya nne ya msimamo wa ligi, ipo visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi ya muda mfupi huku Azam ambayo inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 25, ikiwa imejichimbia Tanga kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally, amefunguka kuwa kocha Kerr hataki mchezo katika mazoezi kwa wachezaji wake kufuatia kuwapa mazoezi ya nguvu asubuhi na jioni, lengo likiwa ni kukiimarisha kikosi na kuwa na ushindani katika mechi dhidi ya Azam pamoja na mechi nyingine za ligi kuu.

“Hapa kwetu kazi tu, kocha hataki mchezo, mazoezi anayowapatia wachezaji si ya kawaida, lengo letu ni kuhakikisha timu inakuwa vizuri katika mechi yetu dhidi ya Azam na ligi kwa jumla.

“Tunahitaji kuwa na kikosi bora na si kwamba tunajiandaa kwa ajili ya Azam pekee, bali tunahitaji kuhakikisha tunashinda kila mchezo uliopo mbele yetu ili kujiweka katika nafasi nzuri,” alisema Abbas.

Kilichoipeleka Azam FC Tanga Chafahamika
Mwandishi Mkongwe Wa Michezo Afariki Dunia