Baada ya kufanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuing’oa Horseed FC ya Somalia, Azam FC wameweka hadharani mipango na mikakati yao.
Azam FC ilisonga mbele mwishoni mwa juma lililopita baada ya kuibanjua Horseed FC ya Somalia bao 1-0 kwenye mchezo wa mkondo wa pili, na kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Mchezo wa mkondo wa kwanza Azam FC ilichomoza na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Horseed FC.
Kocha msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati amesema hawana budi kuanza maandalizi ya kuelekea mchezo wa hatua ya kwanza ya michuano hiyo ya kimataifa, ambapo watacheza dhidi ya Pyramid ya Misri.
“Bado kazi haijaisha kwani tunaendelea na mashindano na tuna kazi nyingine ya kufanya mbele ya wapinzani wetu, kikubwa ni kuona kwamba katika michezo yetu inayofuata tunapata ushindi na kufikia malengo yetu ya kufika hatua ya makundi.”
“Hautaweza kufika katika hatua hiyo ikiwa hakuna mpango wa kushinda michezo yetu inayofuata, lazima yale makosa ambayo tumeyafanya katika michezo iliyopita tuyafanyie kazi,” amesema Bahati.
Azam FC wataanzia nyumbani jijini Dar es salaam Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Pyramid FC Oktoba 15-17 mwaka huu 2021, kabla ya kusafiriki kuelekea Cairo kucheza mchezo wa mkondo wa pili kati ya Oktoba 22–24 , utakaoamua hatma yao ya kusonga mbele.