Uongozi wa klabu bingwa Afrika mashariki na kati Azam FC umekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kufukuzwa kwa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Abdul Mohammed.
Taarifa za kutimuliwa kwa kiongozi huyo, zilianza kuchukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii jana usiku, ambapo zilieleza kuwa, Abdul Mohamed amelazimika kuondolewa klabuni hapo kufuatia mwenendo mbovu wa kikosi cha Azam FC.
Mapema hii leo mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Azam FC, Jaffary Idd Maganga alizungumza na waandishi wa habari na kusema hakuna ukweli wa taarifa hizo, na kama zitakuwepo zitafikishwa katika vyombo vyao vya habari kwa njia maalum.
Amesema hakuna mabadiliko yoyote ya kiuongozi mpaka sasa, na idara yake haijafahamishwa lolote kuhusu mwenendo wa jambo hilo, ambalo amedai limepikwa na baadhi ya watu wasioitakia mema Azam FC.
“Suala la afisa mtendaji mkuu wa Azam FC Abdul Mohammed sijaambiwa chochote na uongozi wa juu, hivyo siwezi kulisemea kwa kuwa halijaletwa kwangu,” alisema Jaffary
Abdul Mohamed aliteuliwa kushika wadhifa wa afisa mtendaji mkuu wa Azam FC mwaka jana 2017, baada ya kuondoka kwa Saad Kawemba.