Mabingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania Bara Azam FC, wameendelea kuomba ridhaa kwa mamlaka za soka nchini kuongeza nafasi za mabadiliko ya wachezaji uwanjani kwa timu moja, kutoka watatu hadi watano.
Uongozi wa Azam FC umeendelea kufanya hivyo, kufuatia shinikizo wanalolipata kutoka kwenye benchi lao la ufundi, linaloongozwa na kocha Aristica Cioaba ambaye aliwasili nchini mwanzoni mwa juma hili akitokea kwao Romania.
Cioaba amesema kuwa, uamuzi huo utakuwa na tija kwa maslahi ya soka la Tanzania na kulinda usalama na afya za wachezaji, hasa katika kipindi hiki ambacho timu nyingi zimekua na muda hafifu wa kujiandaa kabla ya kuendelea kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe La Shirikisho.
“Bado napenda kushauri shirikisho lielewe hali yetu makocha kwamba wiki mbili hazitoshi kufanya maandalizi ya kwenda katika michezo rasmi baada ya kusimama kwa miezi miwili.”
“Baadhi ya wachezaji wanaweza kupata majeraha hivyo maoni yangu ambayo niliyatoa mwezi mmoja uliopita kwamba angalau itupe hiyo fursa ya kufanya mabadiliko ya wachezaji watano,” alisema Cioaba.
Hii ni mara ya pili kwa Cioaba kutoa ombi hilo, kwani aliwahi kushauri kama hivyo mwezi uliopita, akiwa nchini kwao Romania.
Ombi hilo la Azam limetolewa baada ya bodi ya Ligi Kuu ya England kuamua kuongeza idadi ya nafasi za wachezaji kufanyiwa mabadiliko kutoka watatu hadi watano huku kwenye benchi namba ya wachezaji ikiongezeka kutoka saba hadi tisa.
Katika hatua nyingi, Azam FC leo usiku itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Transit Camp inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa ajili ya kupima ufanisi wa kikosi chake.
Cioaba amesema kuwa shabaha yake ilikuwa ni kucheza dhidi ya timu za Ligi Kuu lakini programu za mazoezi zikatibua uwezekano huo.
“Baada ya siku saba za mazoezi tulijaribu kusaka timu ya kucheza nayo mechi ya kirafiki na meneja wangu alikuwa aliwasiliana na timu za Ligi Kuu. Lakini kila moja imekuwa ikiendelea na programu na nilitamani tucheze ili niwaone wachezaji wako wapi kiufundi na kimbinu ili tufahamu kazi tuliyonayo mbele ya safari,” amesema Cioaba.