Kikosi cha Azam FC kimeanza kujiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaowakutanisha na Simba SC utakaopigwa mapema mwezi Mei.

Azam FC itaikabili Simba SC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Mei 6, kuanzia saa tisa alasiri.

Timu hiyo ambayo ilipumzika kwa siku mbili baada ya kuifunga Ruvu Shooting mabao 2-0 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kukwea mpaka nafasi ya tatu, imerejea kujiwinda na mchezo huo.

Kocha Msaidizi wa Azam, Kali Ongala amesema wanajiandaa wakiwa wanafahamu ni mchezo mgumu mno ulio mbele yao lakini hawana budi kujiandaa kwa nguvu kubwa kuhakikisha wanapata chochote msimu huu.

“Ni mechi ngumu, mechi kubwa tunakwenda kucheza Mtwara na tunaelewa mazingira ya kule na hii siyo kwetu tu, hata Simba watakuwa kwenye mazingira hayohayo.”

“Kila kitu kitakachokuwa kwetu ndio kitakuwa kwa Simba, kwa hiyo ni kujipanga vilivyo, kupambana mpaka mwisho na pengine tunaweza kubadilisha kitu mwisho wa msimu huu,” amesema Ongala

Nusu Fainali ya pili ya ASFC inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa CCM Liti, mkoani Singida Mei 7, baina ya Singida Big Stars dhidi ya mabingwa watetezi, Young Africans. Mchezo wa Fainali utapigwa Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.

Rais Samia aongeza mzigo Simba SC, Young Africans
Beki Wydad AC aichimba mkwara Simba SC