Baada ya kukubali kupoteza mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho ASFC dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC kwa kufungwa bao 1-0, klabu ya Azam FC imetangaza kujipanga kulipa kisasi.
Azam FC wamedhamiria kumaliza machungu yao dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa mwezi Julai, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Thabit Zacharia Zaka Zakazi, amesema wamekubali matokeo ya mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho ASFC na yamewaumiza, lakini wamejipanga kulipiza kisasi kwenye uwanja wao wa nyumbani kupitia mchezo wa Ligi Kuu.
“Tumekubali kufungwa. Tulipoteza umakini tukafungwa goli dakika za mwisho. Pamoja na hayo tulikuwa na uwezo wa kumaliza mchezo mapema. Kuna nafasi ambazo wachezaji wetu walizipata, Salum Aboubakar, Idd Nado na Mudathir Yahaya, walipata nafasi ambazo zingeweza kumaliza mchezo, lakini hatukuzitumia.
“Tunajipanga na mchezo mwingine dhidi ya Simba Julai 14 kwenye Uwanja wetu, Chamazi, nina uhakika tutalipa kisasi. Itakuwa ni mechi ya kisasi. Pia tunahitaji pointi tatu muhimu kwenye Ligi Kuu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri,” amesema Zacharia.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kufikisha alama 64, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 67 huku Mabingwa watetezi Simba SC wakiwa kileleni kwa kuwa na alama 73.