Klabu ya Azam FC imethibitisha kufutwa kwa mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya uliokuwa umepangwa kuchezwa mwishoni mwa juma hili mjini Nairobi-Kenya.
Azam FC ilipanga kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kujiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, ambao utaendelea baada ya Kalenda ya FIFA.
Azam FC imethibitisha kufutwa kwa mchezo huo kupitia vyanzo vyake vya habari, ambapo taarifa rasmi imeeleza: Tumesitisha safari yetu ya kuelekea jijini Nairobi, Kenya kwenda kucheza na Gor Mahia Jumapili hii, kutokana na sababu za kiusalama.
Gor Mahia, ilitualika kwenye mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki uliopangwa kufanyika Uwanja wa Nyayo jijini humo.
Hata hivyo, mchezo wetu mwingine dhidi ya JKU ya Zanzibar, uliopangwa kufanyika kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku, utakuwepo kama kawaida.