Vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC wamejinasibu kupambana kufa na kupona mbele ya Young Africans, watakapokutana kwenye mchezo wa mzunguuko wa 12, keshokutwa Jumatano (Novemba 25) Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Azam FC wamejinasibu kupambana kwenye mchezo huo, huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya KMC FC kwa kufungwa bao moja kwa sifuri juzi Jumamosi (Novemba 21), Uwanja wa Uhuru Dar es salaam.

Mkuu wa Idara ya habari na mawasilino Azam FC, Zakaria Thabit (Zakazakazi) amesema kikosi chao kinaendelea kujiandaa na mchezo huo, huku benchi la ufundi likiyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza walipocheza dhidi ya KMC FC.

Amesema dhamira yao kubwa ni kushinda mchezo dhidi ya Young Africans, na kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, ambao kwa sasa unaonesha wamefungana lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa yanaipa nafasi Azam FC kuongoza.

“Tunapambana siku zote kusaka ushindi, lakini juzi jumamosi haikuwa bahati yetu mbele ya KMC licha ya wachezaji kuonyesha juhudi kubwa, wakati wote wa mchezo.”

“Tunarudi tena Uwanjani keshokutwa Jumatano, tutakua nyumbani Azam Complex Chamazi, tukiwakaribisha Young Africans kuanzia saa 1:00 usiku, naamini  haitakuwa kazi nyepesi, ila tutapambana kupata alama tatu mbele ya wapinzani wetu.”

“Hakuna kingine ambacho kinahitajika ndani ya Uwanja zaidi ya timu kupata alama tatu, maandalizi yapo vizuri na kikosi kipo na morali, mashabiki watupe sapoti,” amesema Zakaria Thabit.

Azam FC wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 25 na mabao yake 18, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 25 ikiwa imefunga mabao 13, huku SImba SC inashika nafasi ya tatu kwa alama 23.

Kwa hesabu hizo, mshindi atakaepatikana kwenye mchezo wa keshokutwa Jumatano, ataongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya alama tatu, lakini matokeo ya sare yataendelea kuibeba Azam FC.

Rais wa CAF aingizwa jela ya soka
Klopp: Mo Salah anaanza mazoezi