Kikosi cha Azam FC bado kipo jijini Arusha na kocha wa timu hiyo, Youssouph Dabo ameweka wazi mipango ya sasa ni kuhakikisha inapata matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu itakapovaana na Singida Fountain Gate ili kuendelea wimbi la ushindi walililoanza nalo kwenye ligi hiyo iliyopo raundi ya tatu.

Timu hiyo ilishinda mechi mbili za awali ikiifunga Tabora United ikiwa pungufu uwanjani kwa mabao 4-0 ikichezwa kwa dakika 15 tu, kisha kuilamba Tanzania Prisons kwa mabao 3-1, itaikaribisha Singida FG kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam katika pambano litakalopigwa Alhamisi ya juma hili.

Dabo amesema kama kocha anaendelea kuhakikisha anawalisha madini mastaa wa timu hiyo ili kuhakikisha wanapata ushindi mbele ya wageni wao hao, kwani anaamini halitakuwa pambano jepesi ikizingatiwa wapinzani wao hao wanatoka kucheza mechi ya kimataifa dhidi ya Future ya Misri.

Singida FG ilikuwa kwenye uwanja huo huo wa Azam Complex jana Jumapili (Septemba 17) kumenyama na Wamisri kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikitoka kuambulia suluhu kwenye michezo miwili ya awali ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons.

“Natambua kwamba tuna mechi muhimu dhidi ya Singida FG kwa kutambua ilo ndio maana nimecheza mechi kadhaa za kirafiki ili kuweza kukiweka kikosi sawa,” amesema Dabo na kuongeza kuwa, mechi mbili za kirafiki walizocheza na Arta Solar ya Djibouti na kuilaza 2-1 kisha kufika jijini Arusha na kuifunga Mbuni kwa mabao 2-0 zimemsaidia kukijenga kikosi kwa kufanyia kazi dosari walizonazo baada ya mechi za ligi.

Dabo alifichua siri ya kwenda Arusha kucheza na Maafande hao ili kuwajenga wachezaji wake uzoefu wa kutumia viwanja vigumu kabla ya kuanza kucheza mechi za ugenini za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu.

Mechi mbili za awali Azam FC ilicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi, uwanja ambao una nyasi bandia na wameshauzoea.

Mashabiki washindwa kumuona Messi
Serikali yakanusha taarifa za uwepo jaribio la mapinduzi