Droo ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) imefanyika leo mbashara kupitia Channel ya Azam Sports na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari na wawakilishi wa vilabu.
Droo hiyo imehusisha jumla ya timu 16 zilizofuzu kutoka raundi ya tatu iliyokuwa na timu 32 ikiwemo KMC ambayo imetoka kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Toto African katika mchezo uliopigwa jana usiku kwenye dimba la Chamazi.
Katika droo hiyo, timu sita zinazoshikilia nafasi ya juu zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilitengewa chungu chake ili zisikutane. Timu hizo ni Yanga, Singida United, Azam FC, Mbao FC, Tanzania Prisons pamoja na Mtibwa Sugar.
Walioendesha zoezi hilo ni wachezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Mwanamtwa Kihwelu na Waziri Mahadhi chini ya usimamizi wa mkurugenzi wa mashindano kutoka TFF, Jemedari Said.
Matokeo ya droo hiyo yanaonesha mabingwa wa msimu wa 2016/17 Yanga SC watakwenda ugenini kuikabili Majimaji FC, huku wababe wa Green Warriors, Singida United wakiwa nyumbani kucheza na Polisi Tanzania na timu pekee ya daraja la tatu ngazi ya mkoa, Buseresere ya Geita ikiwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar.
Buseresere ambayo itatumia Uwanja wa Kahama kama uwanja wake wa nyumbani, imefikia hatua hiyo baada ya kuitupa nje Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara katika mchezo wa raundi ya tatu uliopigwa mwezi Januari kwenye dimba la Kaitaba, Bukoba na pia ndiyo timu pekee hadi sasa iliyocheza mechi nyingi zaidi za kwenye michuano hiyo kwakuwa ilianzia hatua ya awali.
Hizi hapa mechi zote nane ambazo zitapigwa kati ya Februari 22 – 25, mwaka huu:-
Stand United vs Dodoma FC.
JKT Tanzania vs Ndanda FC.
Kiluvya United vs Tanzania Prisons.
KMC vs Azam FC.
Majimaji FC vs Yanga SC.
Singioda United vs Polisi Tanzania.
Njombe Mji vs Mbao FC.
Buseresere vs Mtibwa Sugar.