Klabu ya Azam FC inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara imekumbana na adhabu kutoka kwa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa ligi.
Adhabu hiyo imetangazwa hii leo jijini Dar es salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi, Boniface Wambura ambapo amesema Klabu hiyo imepigwa faini ya shilingi laki 5.
Amesema kuwa baada ya kamati kupokea ripoti ya mechi namba 103 kati ya wenyeji Majimaji FC dhidi ya Azam FC timu ya Azam FC iligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kanuni za ligi kuu.
Aidha, mbali na faini hiyo klabu hiyo pia imetakiwa kuwasilisha ushahidi kuhusu malalamiko yake kwenye mchezo huo ambapo ilidai kutoingia kwenye vyumba hivyo kwasababu vilikuwa vimepuliziwa dawa ambayo ilikuwa inatoa harufu kali.
Hata hivyo, Azam FC leo itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu raundi ya 15. ingawa Jumatano iliyopita waliwasilisha barua TFF wakiomba kubadilishwa mwamuzi ili achezeshe mwingine badala ya Israel Nkongo lakini ombi lao limetupiliwa mbali