Uongozi wa Azam FC umeweka wazi kuwa, kwa sasa hauna mpango wa kumrejesha kwenye benchi la ufundi, Kocha Etiene Ndayiragije baada ya kufutwa kazi na Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ kama Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Azam FC wamelazimika kueleza mpango huo, baada ya kusambaa kwa taarifa ambazo zilieleza kuwa, huenda Kocha huyo kutoka nchini Burundi akarejeshwa kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo ili kuongeza nguvu kwa kusaidiana na Kocha Mkuu, George Lwandamina.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulakarim Amin amesema kwa sasa hawana mpango wa kumrejesha kocha huyo kwenye benchi la ufundi, kwani wanaamini mpango kazi uliowekwa na kocha Lwandamina ambaye akabidhiwa mikoba ya Aristica Cioaba, itafanikiwa mwishoni mwa msimu huu.
“Kwa sasa hakuna mpango wa kumrejesha Ndayiragije kwenye benchi letu la ufundi ambalo lipo chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina.”
“Tunaamini na kuheshimu misingi iliyowekwa na Lwandamina, kwa sababu kazi anayoifanya mpaka sasa sio mbaya na hakuna shaka atafanikisha malengo tunayoyatarajia mwishoni mwa msimu huu.” Amesema Popat.
Kocha Ndayiragije alipewa kibarua cha kuinoa Stars akitokea klabu ya Azam FC na aliteuliwa rasmi kuanza kuinoa timu hiyo Julai 2019, akitokea KMC FC.