BAADA ya kumaliza msimu wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao Azam FC ipo kwenye usajili wa wachezaji wapya na leo imemsajili mshambuliaji Rodgers Kola.
Azam imeingia mkataba wa miaka miwili na mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Zambia kwa usajili huru akitokea Zanaco ya Zambia.
Mshambuliaji huyo mzoefu, mrefu na mwenye umbo kubwa, leo amesaini mkataba mbele ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, utakaomfanya kudumu ndani ya viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2023.
Kola anakuja kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam hilo inayoongozwa na Mzimbabwe Prince Dube na ataanza kuonesha makali yake kuanzia msimu ujao wa 2021/2022.
Wakati Kola akiwa Zanaco msimu uliopita, alifunga jumla ya mabao 14 katika mashindano mbalimbali nchini Zambia ikiwemo ligi na kombe la FC.
Sambamba na Kola, Azam ilishainasa saini ya kiungo mshambuliaji Charles Zulu, raia wa Zambia kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini.
CHANZO: MWANASPOTI