Uongozi wa Azam FC umepanga kufanya usajili wa kishindo katika Dirisha hili Dogo kwa kusajili nyota wenye uwezo huku kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Feisal Salum ‘ Fei Toto’ akipaniwa vilivyo kusainishwa klabuni hapo.

Dirisha Dogo la usajili kwa timu za Ligi Kuu Bara, Championship na First League, limefunguliwa tangu Desemba 16, mwaka huu huku likitarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani.

Kaimu Ofisa Habari wa Azam FC, Hashimu Ibwe, amesema wamepanga kufanya usajili wa kishindo katika dirisha hili dogo ambao utawashangaza watu wote na kudai kuhusu ‘Fei Toto’ wanasubiria kamati kuona itaamua nini.

“Mshindo wa Azam FC katika usajili huu utakuwa mkubwa sana, kocha amepanga kusajili wachezaji wawili ama watatu kwa ukubwa ambao watu hawatotegemea.”

“Tayari Kocha Kali Ongalla amewasilisha ripoti yake siku nne zilizopita na tayari ipo kwenye kamati husika inayoshughulika na masuala ya usajili, wanajaribu kuchanganua kama ni ya kutekeleza moja kwa moja ama kwa asilimia chache, tunasubiria kuona kamati itaamua nini baada ya kuipokea.”

“Fei Toto, Dickson Job ni wachezaji wazuri ambao Azam tumekuwa tukihusishwa nao ama wamekuwa wakitajwa na timu nyingine, wote ni wazuri ambao kila timu ya Ligi Kuu itahitaji kuwa nao.”

“Kwa Tanzania Fei Toto ni mchezaji mzuri sana, kwenye viungo washambuliaji wazuri ni miongoni mwao, hivyo tunasubiria ripoti ya kamati ya usajili kuona itaamua nini kama ni yeye ama ni mchezaji mwingine tusubiri tuone kwa kuwa ni wachezaji wenye mikataba na timu nyingine na tunaheshimu mikataba yao.”

“Januari hii timu zinataka kujivika makoti ya usajili mzuri na kuwa kileleni kwa wakati mmoja, ila nasisitiza ninavyojua mimi Azam inataka kufanya usajili wa kushangaza watu,” amesema Ibwe.

Ancelotti, Guardiola wafikiriwa Brazil
BMTZ wakanusha kukwamisha pambano la Mwakinyo