Klabu ya Azam FC imepata mteremko kwenye michuano ya Kombe la Shirikishio, kufuatia wapinzani wao Horseed FC ya Somalia kuchagua Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kuwa uwanja wao wa nyumbani.

Uongozi wa Horseed FC, umeuchagua Uwanja wa Uhuru, kufuatia hali ya kiusalama nchini Somalia kutoruhusu mchezo wowote wa kimataifa kuichezwa kwa sasa.

Katika mchezo huo wa hatua ya awali, Azam FC itaanzia nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, kisha itaendelea kusalia Dar es salaam kwa maandalizi ya siku chache kabla ya kucheza mchezo wa ugenini Uwanja wa Uhuru dhidi ya wapinzani wao Horseed FC.

Maamuzi ya Horseed FC ya kuchagua kucheza mchezo wa mkondo wa pili nchini Tanzania, yanaipunguzia gharama Azam FC ambayo ilipaswa kufanya safari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kucheza mchezo huo.

Mshindi wa jumla katika mchezo huo wa hatua ya awali Kombe la Shirikisho, atacheza dhidi ya Pyramid ya Misri.

Kwa sasa Azam FC imeweka kambi nchini Zambia, ikijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Mukoko Tonombe: Young Africans itafika fainali Afrika
Thadeo Lwanga kuzikosa Kenya, Mali