Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Azam FC, wameanza mikakati ya kuhakikisha wanashinda mchezo dhidi ya Pyramids FC ya Misri.

Azam FC wataanzia nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam Oktoba 16, huku wakihitaji ushindi utakaowaweka kwenye mzingira mazuri kabla ya kucheza mchezo wa mkondo wa pili ugenini jijini Cairo, Misri.

Kocha Msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati amezungumza kwa niaba ya Bosi wake George Lwandamina, ambapo amesema wapo katika mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanashinda mchezo dhidi ya Pyramids FC.

Amesema wanatambua kikosi cha klabu hiyo ya Misri kina uwezo wa kupambana katika mazingira yoyote barani Afrika, hivyo ni jukumu la benchi la ufundi la Azam FC kubuni mbinu ambazo zitawawezesha kushinda mchezo wa nyumbani kabla ya kwenda ugenini Cairo, Misri.

“Jukumu kubwa lililo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunapambana dhidi ya Pyramids katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, hivyo tunajipanga ili kutimiza wajibu wa kupata ushindi,”

“Tunajua utakuwa mchezo mgumu kwetu kutokana na ubora wa wapinzani wetu lakini tunaamini kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mapambano, tutaanzia nyumbani, hivyo ni lazima tuhakikishe tunapata matokeo mazuri kabla ya mchezo wa marudiano ugenini.” amesema Vivier Bahati.

Azam FC walitinga hatua ya kwanza wa michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Horseed FC ya Somalia jumla ya mabao 4-1, kwenye hatua ya awali ya michuano hiyo.

Masha: Nimeombwa kugombea tena Nyamagana, kuna fitna...
Kennedy ashonwa nyuzi sita