Klabu ya Azam FC imejitoa Rasmi katika mbio za Ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2021/22, baada ya kuangusha alama 08 katika michezo mitatu dhidi ya Biashara United Mara, Coastal Union na Polisi Tanzania.
Kauli ya kujiondoa kwenye mbio hizo imetolewa na Idara ya habari na Mawasilino ya klabu hiyo, inayoongozwa na Thabit Zacharia ‘ZAKAZAKAZI’, kwa kusema hawana nafasi tena kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu na nguvu zao wanazielekeza kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
‘ZAKAZAKAZI’ amesema kimahesabu hawako tena katika mbio za Ubingwa wa Tanzania Bara kutokana na uhalisia wa mambo, lakini haikuwa dhamira yao kuishia njiani kama walivyotangaza.
Amesema walijipanga kufanya vizuri msimu huu ili kurejesha heshima ya kuwa Mabingwa kama walivyofanya msimu wa 2013/14, lakini wamekwama kutokana na mwenendo wa kikosi chao kutoridhisha kwa sasa.
“Kwa namna msimamo wa Ligi Kuu ulivyo na namna timu yetu imecheza hadi sasa, kuweza kusema tunahitaji ubingwa hatuutendei haki mpira, kwa sababu hatma ya ubingwa haiko mikonini mwetu.”
“Ili tuweze kuwa Mabingwa, Jambo la kwanza tushinde michezo yetu yote, Jambo la pili wenzetu wapoteze sana michezo yao, tunaweza kufanya maandalizi kwa ajili ya kushinda michezo yetu yote, lakini hatuwezi kufanya chochote ili wenzetu wapoteze michezo yao, kwa hiyo ubingwa bado upo mbali sana.”
“Tunaweza kufanya kitu katika Kombe la Shirikisho, kwa sababu nafasi ya Ubingwa ipo kwa kila mmoja aliyesalia kwenye Michuano hii tukiwemo sisi, hivyo huko tunaweza kuwaambia mashabiki wetu kuwa kuna jambo tumejipanga nalo.” amesema ‘ZAKAZAKAZI’
Hata Hivyo ‘ZAKAZAKAZI’ amesema kwa sasa wanaendelea kujiandaa na michezo inayowakabili huku wakiwa na dhamira ya kukitengeneza kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ili kuweza kufanikisha azma ya kuwa Mabingwa wa Tanzania Bara.
“Tunaendelea kutengeneza timu yetu, kama utakumbuka hatukuanza vizuri sana msimu huu na haya matokeo yanayotukabili ni yale yale tuliowahi kuyaona huo nyuma, kwa hiyo tuna Project ndefu na bila shaka tutafikia lengo siku zinazokuja.”
Kwa hatua ya kushindwa kuwika katika michezo mitatu mfululizo, Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 25 sawa na Namungo FC, lakini ina uwiyano mdogo wa mabao ya kufungwa na kufunga.