Klabu ya Azam FC imesema dozi za mabao mengi inazotoa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa, itazihamishia kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Klabu hiyo imetoa onyo hilo baada ya ratiba ya Raundi ya pili ya Kombe la FA kutoka, huku Azam FC ikipangwa kucheza na Alliance ya Mwanza katika mechi ambazo zimepangwa kuchezwa Desemba 15 hadi 17.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hasheem Ibwe, amesema baada ya kutoka kwa ratiba hiyo, wameanza kujipanga kikamilifu ili kutwaa Kombe kwa sababu wana historia nzuri, pia ni kombe ambalo wana bahati nalo.

“Tunaamini kwamba hili kwanza ni kombe ambalo tumekuwa na wakati mzuri sana nalo, huwa tuna bahati nalo, na timu tunayokwenda kuehezanayo imeshawahi kucheza Ligi Kuu, na kama inavyojua msingi wa timu hiyo ni vijana wa akademi, siyo wa kununua huku na huku, au nje ya nchi, ni wale ambao unawatengeneza wenyewe kutoka shule, hivyo hauwezi kuwa mchezo rahisi.

“Lakini niwaambie tu mashabiki wa Azam, vipigo vinavyotokea huku kwenye Ligi Kuu sasa vitahamia Kombe la FA, dozi ni ile ile, hatuna upendeleo, sindano iliyoshona koti ndiyo itashona ngozi,” ametamba Ibwe.

Msimu uliopita Azam ilitinga Fainali ya Kombe hilo, ikalikosa kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Young Africans, mechi ikichezwa Juni 12 mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Sesanga atangaza kumuunga mkono Katumbi
Wengine wanne wafariki kwa mafuriko