Uongozi wa Azam FC unaamini mengi mazuri yanakuja, baada ya kuanza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21, kwa kuzifunga Polisi Tanzania FC na Coastal Union.
Azam FC walianza kwa kuifunga Polisi Tanzania FC bao moja kwa sifuri kisha wakaibugiza Coastal Union mabao mawili kwa sifuri, michezo yote ikiunguruma kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es salam.
Mkuu wa idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabit Zakaria amesema wanashukuru kuanza ligi vizuri kwa kupata alama sita, huku akiongeza kuwa kilichobaki kwao ni kuendeleza ushindi katika michezo inayofuata.
“Tunashukuru tumeanza ligi kwa ushindi katika michezo yetu miwili mfululizo, ni alama sita muhimu kwetu ambazo tulikuwa tukizihitaji kutokana na malengo ambayo tumejiwekea msimu huu kuwa mabingwa wa ligi kuu.
“Kwa sasa baada ya ushindi huu ni kutafuta mwendelezo wa ushindi katika michezo yetu ijayo ili tujiwekee nafasi ya kuokota pointi nyingi mapema, hakuna kitu kinachoshindikana zaidi ya kujituma kwa wachezaji na kufuatisha maelekezo ya mwalimu,” Amesema Thabit ambaye ni maarufu kwa jina la Zaka Zakazi.
Azam FC mwishoni mwa juma hili watacheza mchezo wao wa kwanza ugenini, kwa kukaribishwa na Mbeya City FC, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Ikumbukwe kuwa Mbeya City walipoteza michezo yao miwili ya mwanzo dhidi ya KMC FC kwa kufungwa mabao manne kwa sifuri, kisha wakakubali kupoteza alama tatu nyingine mbele ya Young Africans kwa kubamizwa bao moja kwa sifuri.