Kikosi cha Azam FC kimewasili salama mjini Cairo, Misri usiku wa kuamkia leo, tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids FC.
Azam FC iliondoka jijini Dar es salaam jana jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, kupitia mjini Adis Ababa imewasili Cairo mishale ya saa saba usiku, ikiwa na deni la kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho.
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam Jumamosi (Oktoba 16), ulishuhudia miamba hiyo ya Azam Complex Chamazi ikishindwa kufurukuta nyumbani, na kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Pyramids FC, ambayo ina uzoefu wa kutosha kwenye michuano ya kimataifa.
Azam FC inahitaji matokeo ya sare ya mabao ama ushindi wowote katika mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumamosi (Oktoba 23), Uwanja wa June 30 kuanzia saa nne usiku, huku wenyeji wao Pyramids FC wakitakiwa kusaka matokeo ya ushindi pekee ambayo yatawasaidia kuvuka hatua ya kwanza na kutinga hatua ya mtoano.