Mabingwa wa kombe la Mapinduzi 2018 Azam FC, wametoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Maji MajiFC katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara uliofanyika leo mchana kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Ruvuma.
Azam FC ndiyo iliyoanza kuliona lango la Majimaji dakika ya 30 kupitia bao safi la winga Joseph Mahundi, aliyeunganisha kiustadi pasi safi ya mshambuliaji Yahya Zayed, bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili Azam FC iliwaingiza nyota kadhaa kwenye dakika tofauti wakiingia viungo Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji Shaaban Idd, ikiwatoa Bernard Arthur, Salmin Hoza na Idd Kipagwile, mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi wakati timu hiyo ilipokuwa ikishambulia.
Dakika ya 73 Majimaji iliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Marcel Boniventure, aliyepiga mpira wa moja kwa moja wa kona uliojaa wavuni na kufanya matokeo kuisha kwa sare hiyo.
Kama Azam FC ingekuwa makini ingeweza kujipatia mabao mengine kupitia nafasi walizopoteza kwenye mchezo huo, kipindi cha kwanza kupitia kwa Bernard Arthur, kipindi cha pili ikipoteza nyingine kwa washambuliaji wake Yahya Zayd, Shaaban Idd na beki Yakubu Mohammed.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mbeya kesho Ijumaa asubuhi tayari kabisa kwenda kucheza na Tanzania Prisons, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sokoine Jumapili hii.