Bodi ya ligi (TPLB) imetangaza maboresho katika zawadi za mchezaji bora wa mwezi wa Ligi kuu Tanzania Bara, ambapo kuanzia sasa, mchezaji bora wa kila mwezi atakuwa akipata tuzo maalum (trophy), fedha taslim shilingi milioni moja pamoja na king’amuzi cha Azam TV.
Afisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura ametoa taarifa hiyo katika mkutano na wanahabari ulifanyika leo katika Ofisi za TFF Dar es Salaam na kurushwa mbashara kupitia channel ya Azam Sports 2 ndani ya Azam TV.
Wambura amesema zawadi zilizoongezwa ni tuzo itakayokuwa ikitolewa na bodi hiyo pamoja na king’amuzi ambacho kitakuwa kikitolewa na Azam TV kama wadhamini wa ligi hiyo upande wa matangazo ya televisheni, huku shilingi milioni moja iliyokuwepo tangu awali, ikiendelea kutolewa na wadhamini wakuu wa ligi ambao ni Vodacom Tanzania.
Amesema tayari zawadi hizo mpya zimeanza kutolewa kwa aliyekuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba, Mudhathir Yahya wa Singida United na kesho (Januari 11, 2018) mchezaji bora wa mwezi Desmba 2017 anatarajia kutangazwa.
Kuhusu tuzo hiyo kuandikwa jina la mchezaji aliyeshinda, Wambura amesema bodi yake italifanyia kazi wazo hilo ambalo limetolewa na mmoja kati ya waandishi waliokuwepo katika mkutano huo.